MASHADA INC

Thursday, December 29, 2011

AZAM FC KUJIPIMA NGUVU NA JKT RUVU KESHO


Zamani miaka ya 70 ilikuwa Brazil Vs Ureno, baadaye ikawa Brazil Vs Argentina, lakini miaka ya 2000 imekuwa Spain Vs Uholanzi na sasa Uruguay imeongezeka. Mara nyingi timu hizi za taifa zinapokutana mashabiki wanaokata tiketi kuona mpambano hutumia dakika 30 za awali kumaliza pesa za viingilio na baada ya hapo huendelea kula faida ya kuchagua kuangalia mpambano huo. Yaani hula faida au ziada.

Ni vigumu sana kwa shabiki kulalamika baada ya mchezo hata kama timu yake itakuwa imefungwa. Baada ya michezo tajwa hapo juu utakuta mashabiki wanafurahia soka lililochezwa na kusema tumefungwa lakini mpira mzuri tumeufaidi kwa maneno mengine tunaweza kusema hawajutii kwenda kiwanjani.

Katika Ngazi ya vilabu, hasa msimu huu nimekuwa nikitamani siku moja katika usiku wa UCL Barcelona ya Spain ikutane na Bayen München ya ujerumani. Nadhani siku hiyo hata kama mechi hiyo itachezwa usiku wa manane ntaamka kuangalia na nadhani sitajutia kukatisha usingizi wangu. Kwa sasa hakuna asiyekubali uwezo wa Barcelona na wafuatiliaji wa kandanda tunajua uwezo wa Bayern Munchen hivyo basi wengi tungependa kuziona timu hizi zikikutana.

Nchini kwetu licha ya Mashabiki wengi kuwa ni wa ki-itikadi yaani Simba/Yanga lakini wafuatiliaji wa soka la Tanzania wanakiri kwamba Azam FC ndiyo kama Barcelona ya Tanzania kutokana na Uwezo wake wa kupiga pasi na kucheza soka lenye mpangilio. Nafasi hii Azam FC imekuja baada ya kuwazidi uwezo au kuipoka timu ya JKT Ruvu Stars yenye maskani yake Mwenge Mlalakuwa yalipo makao makuu ya jeshi la kujenga Taifa JKT.

Utasema nini kuhusu JKT Ruvu? Au utawatoa kasoro gani vijana hawa wa Charles Kilinda? JKT Ruvu wanajua kuuficha mpira na kama wakikutana na timu isiyojiandaa vema basi watawachezesha shere dk 90. Wachezaji wake wafupi wafupi lakini wana kasi ya mchezo na mara nyingi wamekuwa wakifunga magoli mazuri ambayo mtaani huwa tunayaita magoli ya Kideoni.

Lakini wakati mashabiki wengi wa Tanzania ambao tumezoea mpira wa Butua butua tukiishangaa JKT Ruvu kwa soka lake la uhakika, imeibuka Azam FC chini ya Stewart Hall ambapo kwa sasa ni gumzo kwa kuuficha mpira, kucheza kwa malengo, uwezo wa kuzuia kufungwa na zaidi ya yote kupiga pasi nyingi mithiri Unaiangalia Barcelona ya sasa, Spain ya sasa au Brazil ya miaka ya 70.

Juzi katika mechi kati ya Azam FC na Yanga kocha mkuu wa Yanga Kostadin Papic alifura kwa hasira kiasi cha kukataa kuwapa mikono baadhi ya wachezaji wa Azam FC hasa kiungo Jabir Aziz Stima. Papic alitoa kituko hicho ikiwa ni ishara ya kupagawa kiasi cha kushindwa kujua la kufanya. Azam FC ya sasa ni hatari, ina vijana wenye damu changa ambao wana kiu ya mafanikio na wana uwezo wa hali ya juu ya kusukuma gozi.

Baada ya maelezo haya, webmaster wa www.azamfc.co.tz anakusihi shabiki wa soka kufika Chamazi Stadium ujionee kwa macho yako mpambano wa kukata na shoka kati ya timu mbili bora kabisa nchini kwa sasa Azam FC na JKT Ruvu Stars kesho tarehe 30/12/2011 saa kumi jioni. kiingilio kitakuwa shilingi 1000 mzunguko na 5000 jukwaa kuu

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...