Monday, December 26, 2011

CHELSEA YABANWA MBAVU


Klabu ya soka ya Chelsea, imeshindwa kuutumia uwanja wake wa nyumbani vyema na kuwapa mashabiki wake zawadi ya krismasi, baada ya kubanwa mbavu na Fulham katika mechi ya kwanza ya EPL iliyopigwa siku hii ya zawadi.

Wenyeji, ambao walionekana kuwa katika mudi ya hali ya juu, walishindwa kuonyesha makali yao katika kuwamaliza wageni wao licha ya mashambulizi ya hapa na pale waliyokuwa wakiyasukuma langoni mwa Fulham.

Kipa wa wageni, David Adam Stockdale, alikuwa shujaa katika mechi hiyo baada ya kuokoa michomo mingi toka kwa washambuliaji wa Chelsea, katika mechi hiyo ambayo ilienda mapumziko timu zote zikiwa hazijaweza kuona mlango wa mpinzani wao.

Kipindi cha pili kilianza kwa wenyeji kujipatia bao la mapema kunako dakika ya 47, lililowekwa kimiani na mkali wao toka Hispania, Juan Matta, aliyeuwahi mpira ambao ulikuwa ukimtoka mshambuliaji Fernando Torres, ambaye alikuwa amepokea mpira wa krosi toka kwa Ashley Cole.

Hata hivyo, goli hilo haludumu kwa muda mrefu kwani kunako dakika ya 54, Clint Dempsey, aliwasawazishia wageni kufuatia makosa ya safu ya ulinzi ya Chelsea ambapo mfungaji alifunga bao hilo huku David Luiz na John Terry wakiwa kwenye nafasi ya kuokoa mpira huo.

Kwa sare hiyo, Chelsea ambao wameshashuka dimbani mara 18, wanakuwa wamejikusanyia pointi 34, katika nafasi ya 4, huku Fulham walioshuka dimbani sawa na Chelsea, wakiwa wamejikusanyia pointi 19, kwenye nafasi ya 13.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...