MASHADA INC

Monday, December 26, 2011

BERBATOV ATUPIA 3, MAN CITY NAO WABANWA MBAVU


Dimitar Berbatov, ameiwezesha Man United kuwapa mashabiki wake zawadi ya aina yake ya sikukuu ya X-Mass, baada ya kufunga mabao matatu na kuisaidia timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Wigan, huku mahasimu wao Man City wakibanwa mbavu na kujikuta wakiachia pointi mbili muhimu kuwaponyoka.

Katika mechi iliyopigwa kwenye uwanja wa nyumbani wa United, Ji Sung Park, alianza kuwapa mashabiki wa United kicheko cha siku ya zawadi baada ya kuifungia bao la kwanza kunako dakika ya 8, kabla ya Berbatov, ambaye alikuwa kwenye kiwango kuongeza bao kunako dakika ya 41, na hivyo kufanya mechi hiyo kwenda mapumziko kwa matokeo ya bao 2-0 kwa wenyeji.

M-bulgaria huyo ambaye msimu huu amekuwa na wakati mgumu kwa kukosa namba kwenye kikosi cha Sir Alex Ferguson, aliongeza bao la tatu kwa United likiwa la pili kwake kufunga katika mechi hiyo kunako dakika ya 59, na hatimaye akahitimisha hat-trick yake kwa kufunga bao la tano kwa njia ya mkwaju wa penalti kunako dakika ya 78.

Bao la nne liliwekwa kimiani na Valencia kunako dakika ya 75, na ushindi huo umeifanya United kufikisha pointi 45 sawa na mahasimu wao Man City ambao leo hii wamejikuta wakiachia pointi mbili baada ya kuambulia sare ya bila kufungana dhidi ya West Brom Albion, ambao walokuwa nyumbani kwao.

Timu hizo zina pointi 45 kila moja katika nafasi ya kwanza na ya pili, huku zikipishanishwa na uwiano wa magoli ya kufunga nba kufungwa ambapo City wana uwiano wa juu kuzidi United.

Katika pambano lililopigwa kwenye uwanja wa The Hawthorns, City walioonekana kuwa na hamu ya kuibuka na ushindi ili kuzidi kuwa mbali na wanaowafukuzia, waliambulia hasira na pointi moja baada ya wakali wake kukumbana na kikosi kilichokuwa kwenye kiwango cha aina yake upande wa ulinzi cha West Brom Albion.

Kwenye mechi hiyo ambayo City walikuwa wametawala sehemu kubwa ya mchezo huo, walishindwa kabisa kuifungua ngome ya wenyeji wao na pale walipofanikiwa kufanya hivyo walikumbana na kikwazo cha mlinda mlango Benny Foster, ambaye aliokoa michomo kadhaa ya hatari iliyokuwa imeelekezwa langoni mwake.

Sare hiyo inaweza kuwa kipimo cha juu kabisa cha uwezo wa kocha wa City, ambaye baada ya kufurahia ushindi mfululizo kwenye mechi nyingi za mzunguko wa kwanza wa EPL, amejikuta akikabiliana na vikosi vinavyoonekana kuwa imara sana kwa kadiri ligi inavyoendelea.

Katika mechi zingine zilizopigwa leo, Bolton walijikuta wakiruhusu mabao mawili ya haraka haraka kunako dakika za 69 na 71, yakiwekwa kimiani na Ben Arfa na mkali Demba Ba, na hivyo kuwafanya wageni katika mechi hiyo, Newcastle, wakiibuka na ushindi wa bao 2-0.

Liverpool nao wameambiulia sare ya bao 1-1 dhidi ya Blackburn, huku Sunderland waliokuwa nyumbani nao wakitoka sare ya 1-1 dhidi ya Everton.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...