MASHADA INC

Tuesday, July 17, 2012

SIMBA SC KUVUNA KAPU LA MABAO TAIFA LEO?


MABINGWA wa Tanzania, Simba SC leo wanatupa karata yao ya pili katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame, kwa kumenyana na Ports ya Djibouti kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba inaweza kumkosa winga wake iliyemsajili kutoka Kenya, Mtanzania Salim Kinje ambaye ni majeruhi, lakini hiyo inaweza kutoa fursa kwa Uhuru Suleiman au Kiggi Makassy kuibukia uwanjani tangu sekunde ya kwanza, badala ya kutokea benchi kama ilivyoezoeleka.

Daktari wa Simba SC, Cossmas Kapinga alisema kwamba, Kinje aliumia misuli kwenye mechi na Azam, Fainali ya Kombe la Urafiki wiki iliyopita na pamoja ya kujilazimisha kuendelea kucheza, lakini imefikia wakati anahitaji mapumziko.

Kapinga alisema jana Kinje alishindwa kabisa kufanya mazoezi ya pamoja na wenzake na ikabidi afanye mazoezi maalum ya peke yake kulingana na maumivu yake. Kapinga amethibitisha Kinje hatacheza Jumatano ya leo na Ports katika mechi ambayo Wekundu wa Msimbazi, wanatakiwa lazima kushinda ili kufufua matumaini ya kuingia Robo Fainali ya michuano hiyo, baada ya kuanza vibaya jana kwa kufungwa 2-0 na URA ya Uganda.

Ports walifungwa mabao 7-0 na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika mechi ya kwanza na inawezekana Wekundu wa Msimbazi nao wakavuna karamu ya mabao, kama wapinzani wao wa jadi, Yanga SC jana.

Jana Yanga waliifunga Waw El Salaam ya Sudan Kusini mabao 7-1 katika mchezo ambao wangeweza kupata mabao hata mara mbili ya hayo, kama safu yake ya ushambuliaji ingekuwa makini na tulivu. Waw Salaam walifungwa 7-0 na APR kwenye mechi yao ya kwanza.

HABARI KWA HISANI YA BIN ZUBEIRY 

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...