Kikosi cha Yanga |
Na Prince Akbar
HATIMAYE pazia la michuano ya Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame, linapenuliwa leo, kwa mchezo kati ya mabingwa watetezi, Yanga SC dhidi ya Atletico ya Burundi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam saa 10:00 jioni. Mabingwa hao mara nne wa michuano hiyo, wanaingia kwenye mchezo wa leo, wiki moja tu tangu wapate kocha mpya, Mbelgiji Tom Saintfiet ambaye ni juzi tu alitaja wachezaji 20 atakaowatumia kwenye michuano hiyo. Saintfiet aliwaacha kwenye kikosi chake wachezaji watatu nyota na chipukizi, Omega Seme, Simon Msuva na Frank Damayo kwa sababu watakuwa na majukumu ya kitaifa kwa muda mrefu. Aidha, pia aliwaacha beki mkongwe na Nahodha Nsajigwa Shadrack na kiungo Nurdin Bakari. Saintfiet alisema kwamba Omega, Msuva na Damayo watakuwa na timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, inayojiandaa na mechi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika Julai 29 dhidi ya Nigeria.
Kocha wa Yanga Tom Saintfiet |
Mtakatifu Tom alisema falsafa yake ni ushindi iwe wa 1-0 au 5-0 na timu inayoshinda ni ile ambayo kwanza inajilinda vizuri. Hivyo wana Yanga waende uwanjani na leo, wakitarajiwa kuendelea kuona timu yao ikipaki basi na hawana budi kuuvmilia mfumo huo, kwa sababu Tom anataka uzoeleke ili autumie kwa ufanisi baadaye kwenye michuano mikubwa ya Afrika. Tom alitolea mfano mafanikio ya Chelsea msimu uliopita kutokana na mfumo huo, uliowawezesha kuving’oa vigogo wakiwemo waliokuwa mabingwa watetezi Barcelona kabla ya kuifunga Barcelona kwenye fainali na kubeba ndoo ya Ulaya. Mchezo kati ya Yanga na Atlecito, utatanguliwa na mechi baina ya mabingwa wa zamani wa michuano hiyo, APR ya Rwanda dhidi ya Waw Salaam. KIKOSI CHA YANGA KAGAME; Makipa; Yaw Berko na Ally Mustafa ‘Barthez’ Mabeki; Juma Abdul, David Luhende, Kelvin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Godfrey Taita, Ladislaus Mbogo, Oscar Joshua na Stefano Mwasyika Viungo; Athumani Iddi ‘Chuji’, Rashid Gumbo, Juma Seif ‘Kijiko’, Haruna Niyonzima, Shamte Ally, Nizar Khalfan na Idrisa Assenga. Washambuliaji; Said Bahanuzi, Hamisi Kiiza na Jerry Tegete.
HABARI kwa hisani ya BIN ZUBEIRY
No comments:
Post a Comment