MABINGWA wa soka Afrika Mashariki na Kati, Yanga SC Jumatano ijayo wataondoka Dar es Salaam kwenda Kigali, Rwanda kuweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Habari za ndani kutoka Yanga zimesema kwamba maandalizi yote ya safari hiyo yamekwishakamilika na klabu itakuwa huko kwa takriban wiki mbili ikijifua sambamba na kucheza mechi za kirafiki dhidi ya timu tishio za huko.
Miongoni mwa timu zitakazocheza mechi za kirafiki na mabingwa hao wa Kombe la Kagame ni APR, Rayon, Atracao na Polisi, ambazo ndizo timu tishio nchini humo. Mapema jana, kocha wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet alisema anataka mechi mbili kabla ya kutoka nje ya nchi kwenda kuweka kambi fupi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Mtakatifu Tom alisema kwamba mechi dhidi ya timu ya hapa nyumbani na nyingine dhidi ya timu ya nje na baada ya hapo atakuwa tayari kwa safari ya nje nchi na Katibu wa Yanga, Celestine Mwesigwa alisema wanaweza kucheza na African Lyon ya Dar es Salaam na AFC Leopard ya Kenya. Akiwa anaingia mwezi wa pili tangu aanze kazi Yanga, tayari Tom amekwishaweka Kombe moja kwenye kabati la mataji la Yanga, ambalo ni la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame. Yanga ilitwaa Kombe la Kagame kwa mara ya pili mfululizo wiki mbili zilizopita, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kuifunga Azam FC mabao 2-0, ambayo yalitiwa kimiani na Hamisi Kiiza ‘Diego Milito’ na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
Aidha, kwa kutwaa Kombe hilo chini ya Mbelgiji huyo, Yanga imeendeleza rekodi yake ya kutwaa mataji ya michuano hiyo, chini ya makocha wa kigeni baada ya mwaka 1975 kuchukua chini ya Tambwe Leya aliyekuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania, (sasa marehemu), 1993 chini ya Nzoyisaba Tauzany aliyekuwa raia wa Burundi kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania, mwaka 1999 chini ya Raoul Shungu wa DRC na mwaka jana chini ya Mganda, Sam Timbe.
No comments:
Post a Comment