MADIWANI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamesusia uchaguzi wa Naibu Meya Halmashauri ya Manispaa ya Arusha na kuendelea na msimamo wao wa kutomtambua Meya wa Jiji hilo, Gaudence Lyimo na kuiomba serikali uchaguzi wa meya huo urudiwe upya.
Kwa mujibu wa Meya, Lyimo ambaye jana alikuwa akifungua kikao cha baraza la madiwani kabla ya kuanza ajenda mbalimbali za kikao hicho alisema anashangaa ni kwanini madiwani wa Chadema wasuse kikao hicho wakati walikubali muafaka na kumtambua yeye kama meya.
Pia alisema awali madiwani hao walikubali muafaka ili wawaletee maendeleo wananchi lakini alihoji watu hao hao waliokubali muafaka leo hii wanasusia vikao na kumtishia maisha huku wengine wakisema hawamtambui yeye kama Meya na kususia uchaguzi wa Naibu Meya ambaye alitakiwa kutoka ndani ya Chadema.
Lyimo, alisema kuwa kikao hicho kilikuwa na ajenda tatu muhimu ambazo ni kuchagua wenyeviti wa kamati mbalimbali, kupitia taarifa za mapato na matumizi pamoja na uchaguzi wa Naibu Meya, ambaye alitakiwa kutoka Chadema, lakini cha ajabu chama hicho hawajaleta jina wala kuhudhuria kikao hicho.
Alisema kutokana na madiwani wa Chadema ambao ni saba kususia kikao hicho walikubaliana na madiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuachana na ajenda hiyo mpaka kikao cha dharura kitakapoitwa cha kujadili suala hilo.
“Kikao hiki kina washiriki 23 ambapo watano kati yao ni wabunge na 18 ni Madiwani, ila kwa leo wapo madiwani 12 tumefika nusu ya kolamu, ila madiwani wa chadema wameandika barua na kueleza sababu zao za msingi za kususia kikao hiki kuwa wanataka uchaguzi wa Meya ufanyike tena na kuitaka serikali kufanya kukubali uchaguzi urudiwe ili apatikane Meya halali ndipo wao washiriki” .
Alisema barua hiyo waliyoandika Chadema na kuipeleka kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Arusha, pia ilikuwa na vitisho vya kutisha watu maisha, iwapo hawatafanya uchaguzi wa meya, jambo ambalo siyo halali.
Alisema kuwa anakishangaa chama hicho, iwapo kama wameona hawakutendewa haki, ipo sehemu ya kukimbilia mahakamani, ambako hawataki kwenda badala yake wanagoma na kuwatishia watu maisha ni mungu pekee ndiye anayekuwa mlinzi wa watu aliyewaumba.
Lyimo alisema anakumbuka walifanya kikao Juni 20 mwaka jana 2011 na pande hizo mbili na kukubaliana muafaka na kuwapa nafasi ya Naibu Meya Chadema, ila anashangaa kuona wamegeuka makubaliano hayo.
Alisema kikubwa kilichopo kuwaletea wananchi maendeleo na siyo kulumbana, kwa sababu hawakuchaguliwa kuendesha malumbano.
SOURCE;http://www.habarileo.co.tz
No comments:
Post a Comment