KOCHA Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic amekiri kuwepo kwa pengo la mshambuliaji wa kutumainiwa wa klabu hiyo, Emmanuel Okwi kwenye kikosi cha chao kinachoshiriki mashindano ya Kombe la Kagame.
Ikielekea kwenye mchezo wa robo fainali dhidi ya Azam Fc ya Dar es salaam, kocha huyo kutoka Serbia alikiri kuwepo pengo la mshambuliaji huyo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
“Tangu kuondoka kwa Okwi tumejikuta kwenye wakati mgumu kuziba pengo lake, tunajaribu kumtengeneza Okwi mwingine lakini inakuwa ngumu,” alisema Milovan.
Okwi mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda mwenye kipaji cha hali ya juu cha kupiga chenga za maudhi, kutengeneza na kufunga mabao kwa sasa yuko Austria akifanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa nchini humo na tokea kuondoka kwake kumekuwa na ubunifu mdogo wa kutengeneza na kufunga mabao ndani ya kikosi hicho.
Pamoja na tatizo hilo, Milovan aliwaambia waandishi wa habari kuwa kikosi cha timu hiyo kinaendelea kuimarika tokea mechi ya kwanza mpaka mechi zilizofuata.
Alisema kikosi chake kinakabiliwa na majeruhi ambaye ni beki wa kushoto Amir Maftah na hatashiriki tena mashindano hayo, pia beki kiraka Shomari Kapombe naye anasumbuliwa na kifundo cha mguu na ana hatihati ya kucheza.
Milovan alisema wachezaji waliobakia wa timu hiyo wako kwenye hali nzuri na wanaweza kucheza kulingana na atakavyoona. Simba imecheza mechi tatu, ambapo kati ya hizo imefungwa mabao 2-0 na URA ya Uganda, imetoa sare ya moja moja na VITA ya Congo na kuifunga Ports ya Djibout kwa mabao 3-0 kwenye mchezo wake uliofuata.
No comments:
Post a Comment