BI. Harusi mtarajiwa, Elizabeth Terezia (32), mkazi wa Mbezi Beach, Kinondoni jijini Dar es Salaam amebakwa, ameuawa kikatili na watu wasiojulikana wakati akitoka katika Kanisa la Ufufuo na Uzima, Kawe, Dar linaloongozwa na Mchungaji Kiongozi Josephat Gwajima,
Kwa mujibu wa bwana harusi mtarajiwa, Edefonce Sikwembe (42) ambaye ni mkazi wa Kunduchi, Dar tukio hilo la kinyama lilijiri Oktoba 10, mwaka huu majira ya usiku wakati Elizabeth akirudi nyumbani kutokea kanisani hapo.
“Siku ya tukio tulikuwa katika viwanja vya kanisa la Gwajima, nilimpigia simu mwenzangu kumwambia nakwenda nyumbani kuandaa biashara ambayo ningeifanye kesho yake,” alisema Sikwembe.
Jeneza lenye mwili wa marehemu Elizabeth Terezia likiwa mbele ya waombolezaji.
---------------------------
“Kwa maana hiyo yeye nilimwacha kanisani. Saa 2:30 usiku nikampigia tena simu kutaka kujua alipo, akaniambia yupo njiani anaelekea nyumbani kwao.
“Saa 3:00 usiku nilimpigia tena, maana ilikuwa kawaida yangu akiwa nje ya nyumbani kumfuatilia anaporudi ili nijue alipo, lakini cha kushangaza akawa hapatikani, niliamini simu yake iliishiwa chaji.
Marehemu Eliza enzi za uhai wake.
------------------------------------
“Sikuwa na wasiwasi hata kidogo. Hata usingizi wangu usiku haukuwa wa mang’amunga’amu. Alfajiri ya siku iliyofuata nilipoamka nilimpigia simu tena nikiamini mchumba wangu Eliza alichaji simu usiku, lakini bado akawa hapatikani!
“Hata hivyo, niliondoka nyumbani alfajiri hiyohiyo kwenda Buguruni ambako ndiko kuna biashara zangu. Njiani nilimfikiria sana Eliza, si kawaida yake kutopatikana hewani kwa muda wote huo.
“Ilipofika saa 12 asubuhi, shemeji yangu anaitwa Lillian alinipigia simu na kuniambia Eliza tangu alipokwenda kanisani jana yake jioni hajaonekana nyumbani.
Bwana harusi mtarajiwa wa marehemu Eliza, Edefonce Sikwembe (42) akiwa na simanzi.
------------------------------------------
“Kuanzia hapo nilianza kupatwa na wasiwasi, tena mkubwa. Namjua Eliza, si mtu wa kwenda kulala mahali bila taarifa, hasa kwangu,” alisema bwana harusi huyo huku machozi yakimtiririka. Kabla hajaendelea, akasema kwa uchungu na kwa kifupi!
“Da! Inauma sana kwa kweli.”
Akaendelea: “Palepale nilifunga biashara, nikaondoka kwenda kwao ili nikapate maelezo mazuri. Lakini kabla sijafika Mbezi Beach, njiani maeneo ya Afrikana nilikutana na Lillian.
“Tukaamua kwenda kanisani kwa Gwajima kwa ajili ya kuulizia. Njiani akili yangu iliwaza mengi, lakini yale mabaya sikuyapa nafasi na nilimwomba Mungu kwamba kama kuna baya lolote limemfika mpenzi wangu iwe ni filamu na si la kweli.
“Tulifika, mawazo yangu yalitamani tuambiwe Eliza alilala pale kwa ajili ya huduma, lakini ikawa kinyume, tukajibiwa kuwa alipoondoka jana, hakurudi!
Mwili wa marehemu Eliza ukiwa umetelekezwa pembeni yake kukiwa na biblia yake.
--------------------------------------------------
“Kuanzia hapo nilichanganyikiwa, nilikuwa nikitembea eneo la kanisa huku na kule nikiamini nitamwona Eliza wangu, lakini bila mafanikio.
“Nikaenda kuuliza kwa majirani wa maeneo yale lakini majibu yao yalikuwa hawajamuona mtu na aina hiyo. Kuna wakati nilitaka kuamini kwamba, alifichwa eneo lilelile na wafichaji waliniona ninavyohaha kumsaka mchumba wangu.
“Mwishowe, mimi na Lillian tulikwenda Kituo cha Polisi Kawe na baadaye Oysterbay kwa ajili ya kuulizia na kuripoti, nako hakukuwa na taarifa za mchumba wangu.
“Baada ya hapo tuliendelea kuulizia na vituo vingine vya polisi na tulifika Hospitali ya Temeke, Amana na Mwananyamala ambako pia hatukumpata Eliza. Mpaka hapo bado sikuacha kupiga simu yake na iliendelea kutopatikana.” (akatokwa machozi).
Akaendelea: “Siku ya nne tangu kutoweka kwa Eliza, shemeji Lillian alinipigia simu, akaniambia niende nyumbani kwao, nikahisi Eliza ameonekana. Njiani mapigo ya moyo yalikuwa yakienda kwa kasi.
“Nilipokaribia kwao, niliwaona watu wengi wakiwa katika mfereji ambao upo karibu na hapo nyumbani, nikashtuka na kusimama kwanza, kisha nikatembea
“Lakini tayari mwili wangu ukawa unaishiwa nguvu kwani nyuso za watu wale zilikuwa za huzuni tupu. Kusema ukweli japo ni mwanaume, nilishindwa kujizuia, nikakaa chini hasa pia baada ya kuliona ‘Difenda’ la polisi likiwa katika eneo lile.” (Sikwembe akalia tena).
Alipotulia, akaendelea: “Shemeji yangu alinifuata huku akilia na kusema, ‘shemeji hatumaye Elizabeth hatunaye tena duniani.’
Sikwembe alishindwa kusimulia vizuri kutokana na kilio, lakini alisema ilionekana marehemu alitekwa na watu wasiojulikana, wakambaka na kumuua kwa kumnyonga kwa khanga kisha kutuupa mwili wake katika mfereji huo.
Alisema mwili wa marehemu ulikutwa ukielea kwenye maji machafu na umevimba huku nguo yake za ndani ikiwa pembeni yake sanjari na Biblia aliyokuwa nayo kanisani.
“Elizabeth amekufa kifo cha kusikitisha sana, kinaniuma sana, maiti yake ilibidi ichukuliwe kwenye nailoni mpaka Hospitali ya Mwananyamala, lakini uongozi wa hospitali hiyo walisema chumba cha maiti kilijaa hivyo tukampeleka Muhimbili,” alisema mwanaume huyo.
Marehemu alizikwa Oktoba 14, mwaka huu, Mbezi, Dar es Salaam na ilikuwa wafunge ndoa na Edefonce Desemba, mwaka huu na tayari vikao vya harusi vilishaanza kwa pande zote mbili. Mungu ailaze pema peponi roho ya marehemu. Amina.
No comments:
Post a Comment