MASHADA INC

Monday, October 29, 2012

MNYIKA ATOA TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Awali ya yote niwatikie nyinyi
wanahabari kheri ya sikukuu na
kupitia kwenu nifikishe salamu kwa
ndugu zetu waislam na watanzania
wote katika kuadhimisha Iddi Ell-
Hajj.
Tarehe 15 Oktoba 2012 nilitoa
taarifa kwa umma kuwa niliwasilisha
kwa Katibu wa Bunge kusudio la
kuwasilisha Muswada Binafsi wa
Sheria ya Marekebisho ya Sheria za
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (The
Social Security Laws
(Ammendments) Act wa mwaka
2012 kwa hati ya dharura kwa
mujibu wa Kanuni ya 81 ya Kanuni
za Kudumu za Bunge (Toleo la
Mwaka 2007) iwapo Serikali haitatoa
kauli kwa umma ya ratiba ya kupata
mapendekezo toka kwa wadau wa
hifadhi ya jamii pamoja na kamati
husika ya kudumu ya Bunge na
kuwasilisha muswada husika bungeni
kama ilivyoazimiwa bungeni tarehe
6 Julai 2012.
Kufuatia hatua yangu na hatua za
wadau wengine Serikali kinyume na
msimamo wa awali ambalo ulielezwa
na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira
Makongoro Mahanga tarehe 14
October 2012 ambaye alieleza kuwa
marekebisho ya kurejesha fao la
kujitoa hayatafanyika mpaka
mkutano wa kumi wa Bunge mwezi
Februari mwaka 2013; Serikali
imechapa katika gazeti la Serikali
Muswada wa Marekebisho ya Sheria
Mbalimbali na. 40 Juzuu namba 93
ambao katika sehemu ya 6 vifungu
vya 13, 14 na 15 imependekeza
kurejesha fao la kujitoa kwa upande
wa mfuko mmoja wa mashirika ya
umma (PPF) hata hivyo muswada
huo haujawasilishwa kwa hati ya
dharura kama ilivyoazimiwa na
kuahidiwa.
Kwa upande mwingine, sehemu hiyo
ya sita ya muswada huo wa
marekebisho ya sheria mbalimbali
haijakidhi mahitaji na matakwa ya
azimio la bunge la tarehe 6 Agosti
2012 lililoungwa mkono na wabunge
katika kikao cha 41 cha Mkutano wa
Nane wa Bunge na itasababisha
mgogoro mwingine katika ya serikali
na wafanyakazi kwa upande mmoja,
wafanyakazi na waajiri kwa upande
mwingine na kuathiri uchumi wa
nchi na maisha ya wafanyakazi
katika maeneo mbalimbali nchini
kwa kutoresha fao la kujitoa katika
mifuko mingine ikiwemo NSSF, PSPF
na LAPF.
Kwa kuzingatia kuwa Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ibara imeeleza kuwa Rais ndiye
mkuu wa Nchi na Kiongozi wa
Serikali na Ibara ya 34 imeeleza
kwamba mamlaka yote yapo
mikononi mwake na kwamba
madaraka hayo yanaweza
kutekelezwa na watu wengine kwa
niaba yake na kwamba Ibara ya 35
imeeleza bayana kwamba shughuli
zote za serikali zitatekelezwa na
watumishi wa serikali kwa niaba
yake; wakati umefika sasa wa
wafanyakazi na wadau wengine
kuchukua hatua za kuwezesha Rais
kuingilia kati kabla ya mkutano wa
Bunge kuanza tarehe 30 Oktoba
2012 kutumia madaraka na
mamlaka yake kuondoa udhaifu
uliojitokeza wa Waziri wa Kazi na
Ajira Gaudencia Kabaka,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Fredrick Werema na Mkurugenzi wa
Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii (SSRA) Irene Isaka
kutokutekeleza kwa wakati na kwa
ukamilifu mapendekezo na maamuzi
ya Bunge pamoja na ahadi za
Serikali kwa wabunge.
Mosi; Rais azingatie masharti ya
Kanuni za Kudumu za Bunge na
kutia saini hati ya dharura ya
kuwezesha muswada wa
marekebisho ya sheria mbalimbali
wenye vifungu vya nyongeza
vinavyowezesha fao la kujitoa
kurejeshwa kwa mifuko yote
ikiwemo NSSF, PSPF na LAPF
kuwasilishwa bungeni. Kanuni ya 80
Fasili ya 4 inaelekeza kwamba
“Muswada wowote wa sheria wa
Serikali wa dharura hautaingizwa
kwenye shughuli za Bunge bila ya
kuwa na hati iliyowekwa saini na
Rais inayoelekeza kuwa muswada
uliotajwa kwenye hati hiyo ni wa
dharura”.
Iwapo Rais hataweka saini hati ya
dharura au Serikali haitawasilisha
bungeni hoja kwa mujibu wa Kanuni
ya 93 fasili ya 4 bunge litabanwa na
fasili ya 1 ambayo inakataza bunge
kushughulikia hatua zaidi ya moja
katika mkutano mmoja wa bunge;
tafsiri yake ni kwamba sheria hii
itasubiri kupitishwa katika mkutano
wa kumi wa Bunge mwezi Februari
2012 na hivyo wafanyakazi
kuendelea kunyimwa mafao ya
kujitoa kinyume na azimio la Bunge.
Pili, Rais atengue tangazo na agizo la
Mamlaka ya Udhibiti wa Hifadhi ya
Jamii (SSRA) kueleza kuwa “kufuatia
kuanza kutumika kwa Sheria hiyo (ya
13 Aprili 2012) maombi mapya ya
kujitoa yamesitishwa kwa kipindi
cha miezi sita hadi pale miongozo
itakapotolewa ili kuwezesha
Mamlaka na Mifuko ya Hifadhi ya
Jamii kutoa elimu kwa Wadau”
ambalo limesababisha mifuko yote
kuacha kutoa mafao ya kujitoa hata
kwa wafanyakazi .
Hii ni kwa sababu marekebisho ya
sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii
kwa upande wa kusitisha fao la
kujitoa yaliyofanyika tarehe 13
Aprili 2012 yalihusu zaidi Mfuko wa
Mashirika ya Umma (PPF); hivyo
hayakupaswa kabisa kutumika kama
sababu ya kusitisha mafao kwa
mifuko yote ikiwemo NSSF, PSPF na
LAPF na kwa upande mwingine
wafanyakazi wanaodai mafao hayo
kabla ya kujiunga na mifuko hiyo
walijiunga wakiwa wameelezwa kama
kati ya haki na stahili zao ni pamoja
na kupata fao la kujitoa mazingira
yakilazimisha hivyo kabla ya
pensheni ya uzeeni. Hivyo,
kusubiriwa kwa marekebisho ya
sheria hakupaswi kuwa kisingizio
cha kuendelea kusitisha mafao yao
ya kujitoa, ama sivyo Rais aeleze
sababu za ziada za kuzuia mafao ya
kujitoa kwa kuzingatia Taarifa ya
Mkaguzi Mkuu wa Serikali juu ya
uendelevu wa mifuko katika siku
chache zijazo kufuatia kushindwa
kwa makampuni na Serikali yenyewe
iliyokopeshwa na mifuko ya hifadhi
ya jamii kuheshimu matakwa ya
malipo ya mikopo kutoka mifuko
husika ambayo fedha zake
zinatokana na makato ya pensheni
toka kwa wafanyakazi na waajiri.
Rais arejee kumbukumbu rasmi ya
Bunge (Hansard) ya tarehe 7 Agosti
2012 za kikao cha 42 cha Mkutano
wa Nane wa Bunge ambao nilishika
mshahara wa Waziri Bunge lilipokaa
kama kamati na “nilitaka ufafanuzi
wa kisera wa Serikali pamoja na
uamuzi wa kuahidi kwamba kwenye
mkutano wa Bunge ujao italeta
Muswada wa dharura kuhusiana na
Fao la Kujitoa, nilitaka kauli ya
Serikali juu ya agizo lilitolewa na
SSRA la kusitisha utoaji wa mafao ya
kujitoa katika kipindi hiki cha miezi
sita (6) na kuhusiana na wafanyakazi
waliosimamishwa katika hatua ya
kudai hayo mafao.
Sasa iwapo Wizara inatoa kauli ya
kutengua sitisho hilo na vilevile
inatoa kauli ya kutaka kurejeshwa
kwa wafanyakazi waliosimamishwa
katika hatua ya madai ya fao hili la
kujitoa”. Waziri wa Kazi na Ajira
alijibu kuwa “tutalifanyia kazi agizo
hilo”, hata hivyo mpaka sasa agizo
hilo la SSRA halijatenguliwa na
wafanyakazi waliosimamishwa
wengine hawajarudishwa mpaka hivi
sasa na baadhi wamefukuzwa kazi
kabisa kutokana na mgogoro
uliosababishwa na Serikali kusitisha
fao la kujitoa bila kuzingatia haki za
binadamu, mazingira ya ujira nchini
na ushirikishwaji wa wafanyakazi na
wadau wengine muhimu wa hifadhi
ya jamii.
Wenu katika utumishi wa umma,
John John Mnyika (Mb)
26/10/2012


No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...